HABARI

Rais Magufuli awajibu wanaokosoa mpango wa walimu wa sekondari kupelekwa shule ya msingi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewajibu watanzania ambao wanakosoa mpango wa serikali wa kuwapeleka walimu wa sekondari kufundisha shule ya msingi.
 
Rais Magufuli amesema kuwa kitendo hicho ni cha kawaida kwani hakiadhiri mishahara yao bali kinawapa muda mwingi walimu hao kufanya kazi nyingine za ziada.



“Wakati wa Nyerere walikuwa wanachukuliwa walimu wa UPE kwenda kufundisha shule za msingi. Sasa tunachukua wenye digrii. 
"Kikubwa kinachoangaliwa ni mshahara wake tu.. Kwa sababu mshahara unapimwa si kwa vile unafundisha shule ya msingi, ni kutokana na Qualification zako. 
"Tena kule ni kurahisi tu unaweza kufanya na mambo yako mengine.“alisema Rais Magufuli jana Mei 2, 2018 wakati akizungumza na wafanyakazi na wanafunzi  wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, kilichopo mkoani Iringa.



Rais Magufuli alitolea mfano wa nchi zinazotumia Maprofesa kufundisha shule ya msingi;  “Ukienda nchi za Scandinavia utakuta maprofesa ndiyo wanafundisha chekechea, na mishahara yao ni mikubwa kuliko wanaofundisha chuo kikuu. Just mind set.”



Mwezi Februari mwaka huu serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilitangaza kuwa baadhi ya walimu wa masomo ya sanaa kutoka shule za sekondari watapelekwa shule za msingi ili kukidhi mahitaji.

WAZIRI ASEMA SI KILA MTU ANA MAMLAKA KUAGIZA UPIMAJI DNA

Serikali imekataza Mamlaka ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kuruhusu watu au taasisi zisizo na mamlaka kisheria kuwaamuru kupima sampuli za vinasaba (DNA).




Agizo hilo lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, katika hafla ya uzinduzi wa Bodi Tendaji ya GCLA.


Bodi hiyo ina wajumbe saba kutoka Wizara za Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; Mambo ya Ndani ya Nchi, Katiba na Sheria na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).


Dk. Ndugulile ameitaka mamlaka hiyo kutoa elimu kwa jamii kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo, ili kuepuka watu au taasisi kutoa maagizo juu kwa mamlaka hiyo kinyume cha sheria na taratibu.


“Tusiamini kila mtu anajua utaratibu. Tunaweza sasa kuja kuvumbua mambo ambayo hayapo. Si kila mtu anaweza kuamrisha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuchukua vipimo vya DNA, si hivyo kuna taratibu zake,” alisema.


Alisema lazima watu waelezwe taratibu zikoje, nani anawajibika kwenda kupeleka sampuli na nani ana wajibu huo kwa sababu majukumu yake ni ya kisheria.


Dk. Ndugulile alisema katika siku za karibuni suala la kupima vinasaba limezungumziwa sana hali ambayo imezua mkanganyiko kwa jamii, hivyo kuitaka mamlaka hiyo kutimiza wajibu wa kutoa elimu.


Pamoja na kutokumtaja mtu aliyetoa amri ya watu kupimwa DNA, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliwaita watu waliodaiwa kutelekeza watoto kujitokeza.


Baadhi ya watu hao walijitokeza, lakini 90 kati ya wanaume hao, waliwakana watoto waliodaiwa kuwa wamewatelekeza na kutaka waende wakapimwe DNA katika maabara ya Mkemia Mkuu ili kumaliza utata huo.


Katika hatua nyingine, Dk. Ndugulile aliitaka taasisi hiyo kuwa na mkaguzi wa kimataifa wa ubora wa sampuli wanazopima, ili zikubalike kitaifa na kimataifa.


“Lazima muwe na mkaguzi wa kimataifa wa kuthibitisha kile mlichopima kwa sababu taasisi hii ina majukumu ya kisheria ya kuamua ukweli kuhusu sampuli iliyopimwa. Mkisema huu ni unga wa mahindi ilhali tunaona ni dawa za kulevya hatuwezi kupinga,” alisema.


Pia aliitaka mamlaka hiyo kutoa majibu kwa wakati, ili kupunguza kesi zilizopo mahakamani zinazosubiri majibu ya maabara hayo.Alisema, ili kutekeleza agizo hilo, amewataka kuandaa mikataba inayoonyesha kazi itakamilika kwa muda gani pindi wanapopokea sampuli.


“Utakumbuka kuna wakati kesi zilirundikana katika mahakama zetu hivyo mnatakiwa kufanya kazi kwa haraka na kwa wakati na muwe na mikataba inayoonyesha kazi itakamilika kwa muda gani,” alisema.


Pia aliwataka kuwatambua wale wote wanaojihusisha shughuli za kemikali nchini wakiwamo, wauzaji, wanunuzi na wanaozitumia kwa ajili ya kupunguza matukio ya uhalifu nchini.


Kadhalika aliwataka kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi na Mazingira (NEMC) kuthibiti majitaka katika viwanda, ili kuepusha madhara kwa watu.


“Sijawasikia mkipima maji taka yanayotiririka viwandani mmekaa kimya kama si wajibu wenu, hakikisheni mnashirikiana nao na kuchukua sampuli nyie wenyewe mpime na mtoe majibu,” alisema.


Naye Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, alisema GCLA inakabiliwa na uhaba wa watumishi takribani 200 na pia uchakavu wa mitambo ya kimaabara.


Dk. Mafumuko pia alisema fedha za bajeti ya serikali ya mwaka 2017/18 zilizotengwa kwa ajili ya kununua mitambo na vifaa vya maabara hiyo hazijatoka hadi sasa hali ambayo inawafanya kushindwa kutekeleza majukumu yako kikamilifu.


Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Ester Jason, aliahidi kuisumbua wizara hiyo kuhusu kutekeleza majukumu ya mamlaka ikiwa ni pamoja na kutoa fedha mapema iwezekanayo.

Mafuriko yakwamisha ‘Mwendokasi’ Dar

Kampuni ya mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (UDA-RT) imesitisha huduma ya usafiri kuanzia saa sita mchana leo, Ijumaa, baada ya Barabara ya Morogoro kufungwa eneo la Jangwani ambalo limefurika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano UDART, Deus Bugaywa ambayo imesambazwa kwa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, maji yamejaa katika eneo la Jangwani na kupita juu ya Daraja la Mto Msimbazi. Mkuu huyo amewataarifu wateja wa huduma hiyo ya usafiri kuwa maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam yanaendelea kupata huduma ya mabasi ya UDART kama kawaida kwa kuwa mvua hazijasababisha athari sehemu hizo.
“Kwa sasa huduma zinatolewa kwa njia za Mbezi-Kimara, Kimara-Morocco, Kimara-Magomeni Mapipa, Kivukoni-Muhimbili, Gerezani-Kivukoni na Gerezani-Muhimbili. Huku taarifa hiyo ikuomba radhi wateja kutokana na usumbufu uliojitokeza, UDART imewahakikishia kuwa huduma hizo zitarejea pindi barabara itakapofunguliwa.

Comments

Popular posts from this blog